JINA LA RIWAYA: MAPENZI YA GIZA
MTUNZI: JUSTIN BARUTI
SMS & WHATSAPP: 0752474397
UTANGULIZI
Mapenzi ni safari isiyotabirika, yenye mikondo ya furaha, huzuni na maamuzi mazito. Ni safari inayoweza kukuinua juu ya mawingu au kukusukuma chini kabisa. Lakini je, tunaelewa gharama ya mapenzi tunayoyachagua? Katika kila mahusiano kuna ishara nyekundu, njano au kijani. Swali ni: Je, tunazitambua ishara hizo kabla hatujaumia au tunasubiri mpaka tumekwama kabisa? "Mapenzi ya Giza" ni simulizi ya maisha, yanayokusihi utafakari kabla ya kujitosa zaidi
*SEHEMU YA KWANZA*
Mchana wa joto jijini Dar es Salaam mitaa ilikuwa imejaa kelele za magari, sauti za wauza bidhaa wakipaza sauti zao na hewa ya pilikapilika za kila siku. Rehema alikuwa ameketi ndani ya mgahawa wa kawaida macho yake yakitazama kupitia dirisha kubwa lililoelekea barabarani. Alikuwa amezoea kuja hapa kila siku baada ya kazi akipenda utulivu wa mahali hapa na kahawa ya bei nafuu lakini yenye ladha
“Nitumie cappuccino na keki ya vanilla” alimuambia mhudumu kwa sauti tulivu
Dakika chache baadae alihisi kivuli kikubwa kikisimama karibu nae
“Samahani hiki kiti ni huru” sauti nzito ya kiume ilisikika
Alipoangalia juu alimkuta mwanaume mrefu aliyevaa suti ya gharama na tabasamu la kutozuia
“Ndio unaweza kukaa” Rehema alijibu kwa aibu kidogo akihisi kwamba macho yake yalikuwa yanamulika kwa muda mrefu zaidi ya kawaida
“Naona mgahawa huu umekuwa maarufu siku hizi” alisema mwanaume huyo akiangalia pande zote
“Ni mahali pazuri kwa mtu anayetaka utulivu” Rehema alijibu akirudisha macho yake kwenye kikombe chake cha kahawa
“Sahihi kabisa. Samahani, sikujitambulisha...jina langu naitwa Dennis” alisema huku akinyoosha mkono wake
Rehema alisita kwa sekunde kisha akakubali kushikana nae mkono
“Rehema” alijibu akimwambia Dennis jina lake
Majibizano yalifuata kwa upole Dennis alionekana kuwa na haiba ya kipekee akichanganya maneno yake kwa ustadi na ucheshi wa kuvutia. Ilikuwa ni mara ya kwanza baada ya muda mrefu kwa Rehema kuhisi kupendelewa na mtu hasa mtu aliyekuwa na sura na mavazi kama Dennis
Siku hiyo iliisha kwa Dennis kumuomba namba ya simu. Rehema alisitasita lakini mwishowe akakubali
"Pengine ni mwanzo wa kitu kizuri" alijisemea moyoni
Baada ya siku chache za mazungumzo kupitia simu na SMS za kawaida, Dennis alimualika Rehema kwa chakula cha jioni kwenye hoteli maarufu. Hapo ndipo alipoanza kugundua upande wa kifahari wa maisha ya Dennis magari ya gharama kubwa, mazungumzo ya kibiashara na marafiki wenye ushawishi lakini kulikuwa na kitu ndani yake kilichomsumbua
Licha ya haiba ya kuvutia, kulikuwa na ukimya wa ajabu uliojaa maswali ambayo Dennis hakuonekana tayari kujibu
“Unapenda kufanya nini mbali na kazi yako Dennis” Rehema aliuliza wakati wa chakula cha jioni
“Niko bize sana kwa mambo mengine” alijibu Dennis huku akiangalia simu yake
“Lakini kila mtu anahitaji muda wa kupumzika si ndio?” Rehema alisisitiza
Dennis alitabasamu kwa upole
“Labda siku moja nitakuonyesha upande wangu wa kawaida..kwa sasa, acha tujifurahishe na sasa”
Maneno hayo yalionekana kumaliza mjadala. Dennis alikuwa mjanja wa kugeuza mada jambo ambalo Rehema alilitambua lakini hakulitilia maanani. Hii ilikuwa mara ya kwanza katika muda mrefu kwa mtu kumfanya ajisikie maalum na hakutaka kuiharibu
Siku ziliendelea na mahusiano yao yalizidi kushika kasi. Dennis alianza kumzawadia zawadi za ghafla mikufu, simu mpya na hata safari fupi za kitalii. Wakati huo marafiki wa Rehema walianza kuonyesha wasiwasi wao
“Huyu Dennis ni mzuri sana, lakini unajua nini kuhusu maisha yake ya zamani” rafiki yake bora Zawadi aliuliza
“Zawadi, si kila kitu kinahitaji uchunguzi wa kina. Yeye ni mtu mzuri na kwa kweli najisikia furaha nae” Rehema alijibu
“Usikubali kila kitu kinachoonekana juu juu Rehema. Dunia ya sasa ni ya hatari” Zawadi alionya
Lakini Rehema hakuwa tayari kusikiliza, Dennis alikuwa amejaa kila kitu alichohisi alikuwa amekikosa maishani upendo, heshima na maisha yenye ladha ya kipekee
**************************
Kadiri muda ulivyopita, ishara za hatari zilianza kujitokeza polepole lakini kama alama kwenye barabara ya jiji zilizofunikwa na majani yaliyokusanywa na upepo, Rehema hakuziona mapema. Dennis hakuwa tu mfanyabiashara; kulikuwa na kitu kingine zaidi siri ambayo ingeweza kubadilisha kila kitu
*USIKOSE SEHEMU YA PILI*
*JE REHEMA ATAGUNDUA ISHARA ZA KWANZA ZA GIZA KATIKA MAISHA YA DENNIS?!*
Tags
Riwaya